Ijumaa, 21 Julai 2017

HATIMAYE BWAWA LA NYUMBA YA MUNGU LAFUNGULIWA


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel   N. Bendera akishirikiana na Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro Mhe. Anna Mghwira wameongoza kikao cha ujirani mwema cha kujadili hatua waliyofikia kulinda Mazingira na viumbe hai hasa samaki katika Bwawa la Nyumba ya Mungu lililofungwa mwezi  Mei 2016 ili kuzuia uvuvi haramu na kuruhusu samaki kuzaliana katika Bwawa hilo.
Aidha, baada ya Kikao hicho kilichofanyika Mkoani Kilimanjaro katika ukumbi wa Mikutano wa Wilaya ya Mwanga, ujulikanao kama Teachers  Learning Centre na kujumuisha Kamati za Ulinzi na Usalama za pande zote mbili, wataalamu mbalimbali na baadhi ya wajumbe kutoka Wilaya ya Simanjiro na mwanga,Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa walikwenda kuongea na wananchi wa kijiji cha nyumba ya Mungu kata ya Ngorika  Wilaya ya Simanjiro ambapo Mheshimiwa Dkt.Bendera alifungua rasmi Bwawa hilo na kuwataka wananchi wa Kijiji hicho kuzingatia maagizo yote ya matumizi ya Bwawa hilo.
Mheshimiwa Dkt.Bendera amesisitiza kuwa kutokana na makubaliano ya kikao cha awali kabla ya Mkutano na wananchi Bwawa hilo litakuwa likifungwa tarehe moja Januari kila mwaka hadi tarehe 30.6 kila mwaka ili kuruhusu samaki kuzaliana.


Maagizo ya Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro na Manyara kuhusu Bwawa la Nyumba ya Mungu.Maagizo ya Waheshimiwa wakuu wa Mikoa ya Manyara na Kilimanjaro kwa Halmashauri za Moshi, Mwanga na Simanjiro katika kusimamia utaratibu wa Bwawa la Nyumba ya Mungu ili shughuli za uvuvi ziwe endelevu na zenye tija.
 •  Uundaji wa kamati za forodha BMU (Beach Management Unit) katika kila forodha/Mialo zinazotambulika na kupewa mafunzo.
 • Wavuvi wote lazima wazingatie taratibu za uvuvi zilizowekwa na vikundi vyao vya BMU katika mwalo/forodha husika.
 • Ni lazima vyombo vyote vya uvuvi (Ngalawa, Mitumbwi nk.) kusajiliwa sambamba na ukaguzi wa zana zote za uvuvi ufanyike.
 • Utoaji wa leseni mbalimbali za uvuvi (vyombo vya uvuvi, leseni za uvuvi na leseni ya biashara ya uvuvi) zitatolewa kwa wale ambao wamekidhi viwango vya kupewa lesseni hizo.
 • Vyombo vyote vya uvuvi (Ngalawa Mitubwi nk.) lazima viegeshwe kwenye forodha husika baada ya shughuli za uvuvi na chombo ambacho kitakutwa nje ya forodha husika kitachukuliwa hatua kali.
 • Wavuvi wote watashusha samaki katika mialo/forodha zinazotambulika rasmi atakayekiuka agizo hili atachukuliwa sheria ikiwa ni pamoja na kutaifishiwa samaki.
 • Wavuvi wote wavue samaki wenye ukubwa kuanzia nyanda tatu na kuendelea kama sheria na taratibu za uvuvi zinavyoelekeza.
 • Mtu yeyote haruhusiwi kumiliki, kutumia au kumwachia mtu mwingine kutumia Kokoro,Chandarua, Katuli, Kimia, kokoro ndogo kwa madhumuni ya uvuvi.
 • Samaki wabichi watasafirishwa ndani ya magari maalumu box board yenye barafu yaliyoandikwa maneno SAMAKI TU/FISH ONLY.
 • Ni marufuku kuchanganya mazao ya samaki pamoja na abiria au mizigo mingine yeyote.
 • Kukata ushuru wa samaki katika sehemu husika.
 • BMU na serikali za vijiji zitawajibika kuthibiti uvuvi haramu katika maeneo yao na pale watakaposhidwa kutekeleza agizo hili Afisa Mtendaji wa kijiji mwenyekiti wa kijiji na mwenyekiti wa kitongoji husika hatua kali za kisheria zitachukiliwa dhidi yao.
 • Hairuhusiwi mtu kumiliki sehemu yeyote ya maji (WERA) na ikibainika hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kuzuiliwa kujihusisha na shughuli za uvuvi pamoja na kifungo cha miezi sita au faini isiopungua milioni moja.
 • Wachuuzi wote na wavuvi watawajibika kulipa ushuru wa samaki. Mchuuzi ambaye atakwepa kulipa ushuru huo pindi akibainika na kukamatwa hatua kali zitachukuliwa ikiwa pamoja na chombo cha usafiri kupigwa faini na pia samaki wake watataifishwa.
 • Wakurugenzi wapeleke nakala ya sheria za uvuvi katika kila ofisi ya Mtendaji wa Kijiji kinachohusika na maeneo ya uvuvi ili kuwaelimisha wananchi.


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni